top of page

Kukiuka Maadili Katika Bima ya Afya.

Updated: Aug 11, 2025

Je unafahamu kuwa kuna baadhi yetu tunakiuka maadili katika matumizi ya bima ya afya? Hatari ya kukiuka maadali katika bima ya afya ni nini?


Maana rahisi ya kukiuka maadali katika bima ya afya ni kufanya matumizi au kutumia bima ya afya au kuendea huduma za afya pasi ulazima wa kufanya hivo kwa sababu tu unamiliki bima ya afya na hautumii pesa yako mfukoni. Tabia hii inaweza kufanywa na mwanabima yaani mgonjwa au mtoa huduma ya afya aidha daktari au kituo cha kutolea huduma.


Kukiuka Maadili kwa Mgonjwa

Kwa kuwa tu mtu ana bima, anatambua kuwa akienda katika kituo cha kutolea huduma za afya hatalipa pesa. Hivo, anadhani kuwa ili kutumia bima yake vema, anaweza kwenda katika kituo cha kutolea huduma za afya bila ya sababu za msingi. Kwa mfano, utasikia mtu anasema “sijatumia bima yangu mida mrefu, ngoja nikafanye chek-up mwili mzima”,  huu msema wa check-up ya mwili mzima maana yake ni kubwa na huenda gharama yake hailingani hata na pesa anayochangia kwenye bima katika kipindi chote cha maisha yake. Utaratibu huu unapelekea matumizi mabaya ya bima na huduma za afya kwa ujumla.


Namna nyingine ni mtu anapofika kituo cha kutolea huduma za afya, anaomba au kulazimisha huduma za ziada ambazo sio lazima kwake kwa wakati huo. Mfano, utaona mgonjwa anafika kwa daktari na kusema “Nimekuja kupima, UTI, malaria, typhoid, na picha ya damu” hata kama daktari hakushauri vipimo hivyo. Ni wazi mgonjwa anatakiwa kusikiza ushauri wa daktari hasa anapokua anatumia bima, ili kulinda mfuko wa bima anaochangia.


Mgonjwa anaingia katika kukiuka maadili ya matumizi ya bima pale analazimisha kupatiwa huduma za kibingwa au ubobezi pasi na ulazima huo. Ngazi za madaktari au matabibu zimeweka kwa makusudi na malengo mazuri kabisa. Baadhi yetu, kwa sababu tu tunatumia bima na hatutoi pesa mfukoni, tunalazimisha kutumia huduma za kibingwa ambazo ni ghali zaidi na zinaugharimu mfuko wa bima.

Kwa mfano, inawezekana kabisa ukiwa na homa au dalili ambazo sio hatari kutumia kituo cha kutolea huduma ngazi ya chini kama vile zahanati au kituo cha afya na vipimo na dawa utazopatiwa zinalingana na atazoandika daktari bingwa wa hospitali ya mkoa au taifa. Kwenda kumuona daktari bingwa katika ngazi ya juu kunauazimu mfuko kulipia huduma kwa gharama zaidi kuliko katika ngazi ya chini unapotibiwa na daktari wa kawaida.


Hali kadhalika, baadhi ya watu wanakiuka maadaili ya bima kwa kutojali afya zao. Mtu anajiingiza katika tabia zinazohatarisha afya yake kama vile unywaji wa pombe, uvutaji sigara, kuendesha vyombo vya moto (magari,pikipiki, n.k) bila umakini kwa sababu hata akipata changamoto ya afya ana bima. Huku ni kukiuka maadili ya matumizi ya bima na kupelekea kugharimu mfuko zaidi.


Kukiuka Maadali kwa Mtoa Huduma

Kwa kiasi kikubwa baadhi ya watoa huduma za afya wamekua wakikiuka maadili ya matumizi ya bima za afya na kupelekea kudhoofisha maendeleo ya mfuko au utoaji wa huduma za afya kwa ujumla. Hii inatokea hasa pale ambapo mtoa huduma analipwa kulingana na idadi au wingi wa huduma anayompatia mteja


Mtoa huduma akilipwa kulingana na huduma anajua kuwa akimpatia huduma nyingi zaidi mgonjwa naye atapata pesa nyingi. Hivo, analazimika kumuandikia vipimo vingi na sawa nyingi hata pale isipohitajika ili tu kufikia malengo ya pesa anazokusudia. Hii inaweza kufanywa na mtu binafsi yaani tabibu, daktari au muuguzi, au kituo cha kutolea huduma kwa ujumla kuwalazimisha wafaya kazi wake kufanya hivo.

Vile vile, mtoa huduma anaweza kushauri mgonjwa atembelee kituo cha kutolea huduma za afya mara kwa mara kwa kujua kuwa, kila hudhurio analipwa. Bila hata mgonjwa kufahamu au kukusudia, analazimika kwenda kituo cha kutolea huduma za afya mara kwa mara, na kuingia gharama ya nauli na muda kwa sababu mtoa huduma anataka kuingiza pesa na kutengeza faida kinyume na maadili.


Madhara ya Kukiuka Maadili Katika Bima ya Afya.

Kwa upeo wa karibu, ni haki ya mtu kutumia bima yake ya afya, japokuwa umakini, ustaarabu, na utashi wa kufikia maleng makubwa zaidi yapewe kipaumbele. Kwa kifupi bima ya afya inatumia mfumo wa mshikamano (solidarity) kwa kuleta makundi mbalimbali pamoja kuchangia huduma za afya. Mwenye kipato kikubwa nachangia zaidi kuliko mwenye kipato kidogo, mwenye magonjwa mengi anachangia kwenye mfuko mmoja na asiyekua na maradhi kabisa, pia mzee anachangia mfuko mmoja na kijana na watoto.


Mfumo huu unasaidia kuweka uwiano wa matumizi kwa wanaotumia bima sana kama vile wazee, watoto na wenye magonjwa ya muda mrefu kuliko wengine. Sasa, endapo matumizi ya bima yatafanyika kwa kukiuka maadili, mfuko utashindwa kuhimili uwiano kati ya michango na matumizi na hata kupelekea kushindwa kutoa huduma bora za faya kwa wahitaji zaidi kikamilifu: machache katika madhara ya kukiuka maadili ya matumizi ya bima ni pamoja na;


  • Kuongeza Gharama Katika Utoaji Huduma

Gharama za matibabu haziishii kwa mfumo kutoa pesa nyingi zaidi wakati wa kukiuka maadili. Bali gharama inaongezeka pia zaidi kwa mgonjwa na mtoa huduma binafsi na kituo cha kutolea huduma za afya kwa ujumla. Kwa mfano, ikiwa mgonjwa au mtoa huduma ameongeza vipimo zaidi kinyume na ilivyotakiwa, mgonjwa ataingia gharama ya kusubiri majibu kwa muda mrefu zaidi na pengine kurejea tena kituoni siku nyingine ili kupata majibu yake. Maana yake ni kwamba amepoteza muda wa uzalishaji na kituo cha huduma za afya kinaingia gharama ya kumuhudumia mgonjwa kwa muda mrefu zaidi ambao ungetumika kuhudumia mteja mwingine.


Kwa mfano huo huo wa vipimo, viwatilifu vinatumika zaidi, na vifaa tiba pia ambavyo vinahitajika kununuliwa tena na pengine kupelekea mfumo mzima wa ugavi kushindwa kukidhi mahitaji hayo na kupelekea gharama zaidi aidha kwa kutafuta vifaa hivo nje ya mfumo husika wa ugavi.


Kubwa zaidi ni kuupelekea mfuko wa bima kutumia pesa nyingi zaidi kwenye kulipia huduma za afya ambazo hazikuwa lazima na kushidwa kufanya maendeleo katika mfumo zima wa afya na hatimaye kugharimu mnyororo wa utoaji wa huduma za afya kwa ujumla.

  • Kusababisha Madhara Kiafya

Kukiuka maadili kama vile kutojali afaya yako binafsi kwa sababu tu una bima kunapelekea hatari zaidi kama vile magonjwa yasioambukiza mfano shinikizo la damu na kisukari. Kwa hakika bimaitalipia huduma za afya kama vile dawa na vipimo, lakini magonjwa haya yana gharama zaidi ya hela za matibabu. Tafiti zinaonyesha kuwa, magnjwa ya muda mrefu yanahusika sana kusababisha msongo wa mawazo na sonona na kupeteza ubora wa maisha.


Kwa mfano mgonjwa akilazwa na kituo cha kutolea huduma kikakiuka maadili kwa kudhani kuwa mgonjwa akiwa wodini siku nyingi zaidi kitaingiza pesa nyingi zaidi, inaweza kupeleka mgonjwa hata kupata magonjwa mengine akiwa hospitalini na kuongeza siku za kulazwa maradufu. Pia, inaweza kupelekea mgonjwa kufanyiwa matibabu hata ambaya haitaji na kumdhuru kiafya.


  • Kupoteza Tija ya Matibabu

Ikiwa mgonjwa anaamua nataka kufaya check-up mwili mzima, analazimisha vipimo ambavyo havihitaji au mtia huduma anamuandikia mgonjwa vipimo na dawa ambazo sio lazima, tija ya matibabu inaondoka. Japokuwa kwa maadili ya kitabibu mgonjwa ana haki na uhuru juu ya huduma anayopatiwa, hana budi kutambua kuwa tabibu ana uelewa na weledi wa kulinda afya yake. Pia, maadili ya kitabibu yanamtaka mtoa huduma kuto sababisha madhara kwa wateja wake ili tiba iwe na tija.


Katika kukiuka maadili ya bima mgonjwa na daktari wanakua nje ya mipaka ya kuhakikisha haki na wajibu wa kila mmoja unakua ndani ya mipaka ya maadili ya matibabu. Hivyo basi, tija ya matibabu na kufuata maadili ya matumizi ya bima ya afya yanaenda sambamba.

Mwisho….

Mifuko ya bima za afya Tanzania iko mingi, haijalishi unatumia Bima ya Afya ya Taifa au aina zingine za bima, misingi ya kukiuka maadili inafanana. Hivyo basi, hakikisha unatumia vema na kwa uadilifu aina yoyote ya bima ya afya ili kulinda mfuko na afya za wahitaji wa huduma za afya zaidi. Hakika mshikamano ndio nguzo ya kuhakikisha kila mmoja wetu anapata matibabu yaliyo bora.


 
 
 

Comments


bottom of page